
Hali hiyo imeathiri abiria 3,000 huku ndege nyingine 15 zilizotarajiwa kutua katika uwanja huo zikielekezwa katika viwanja vya ndege vya Stuttgart, Nuremberg, na Frankfurt.
Kwa mujibu wa taarifa ya usimamizi wa uwanja huo, tukio hilo limeongeza taharuki ya kiusalama, hasa ikizingatiwa kuwa limetokea siku chache tu baada ya viwanja vya ndege vya Denmark na Norway kufungwa kwa muda kutokana na matukio ya aina hiyo ya droni kuonekana katika anga ya nchi hizo.
Mji wa Munich tayari ulikuwa katika hali ya tahadhari mapema wiki hii, baada ya tamasha maarufu la Oktoberfest kusitishwa kwa muda kufuatia tishio la bomu na kugunduliwa kwa vilipuzi katika jengo la makaazi kaskazini mwa mji huo.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameunga mkono pendekezo la kuimarisha ulinzi wa anga wa nchi wanachama dhidi ya tishio la droni, hasa zile zinazodaiwa kuwa za Urusi.