Jumanne , 14th Oct , 2014

Uongozi wa mkoa wa Kigoma nchini Tanzania umesitisha uopoaji wa miili ya watu waliopata ajali baada ya mitumbwi miwili kugongana kijiji cha Kalalangabo kwenye mwambao mwa ziwa Tanganyika wakati watu hao wakitokea kwenye harusi mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali Mstaafu Issa Machibya.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya amesema kuwa vikosi mbalimbali vya ukoaji kwa kushirikiana jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakishirikiana na wananchi wamefanya kazi kubwa ya kuopoa miili kwa kipindi cha siku Tatu mfululizo.

Kanali Machibya amesema jumla ya miili kumi imepatikana katika zoezi hilo la ukoaji lakini hivi sasa wameachia uongozi wa serikali ya kijiji cha kalalangabo kuendelea kutoa taarifa kama kuna miili mingine itakayoibuka kutokana na kuhofiwa kuwa bado miili mingi ipo majini

Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kuacha tabia ya kutumia vyombo visivyo rasmi katika usafiri na ambavyo havijasajiliwa na mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA) pia amewataka wavuvi na wale wenye vyombo majini waache tabia ya kusafirisha abiria kwa kutumia mitumbwi ya kuvulia dagaa ili kuepuka ajali.