Alhamisi , 5th Apr , 2018

Watu wanne wanashikiliwa na Polisi Ngerengere, Mkoani Morogoro wakituhumiwa kuhusika na wizi wa lita 2510 za mafuta aina ya Dizeli kutoka kambi ya ujenzi wa reli ya kisasa Standard Geuge.

Watuhumiwa hao wamekamatwa na polisi kikosi maalumu cha reli nchini kwa kushirikiana na maafisa wa shirika la reli Tanzania ambapo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.

Akizungumza na waandishi wa Habari Kamanda wa Polisi Kikosi Maalumu cha Reli Salum Kisai, amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao itakuwa fundisho kwa watanzania wengine wanaofanya kazi katika mradi huo ili kuweza kulinda mali za mkandarasi na kumaliza kwa mradi huo kwa muda unaotakiwa.

Kwa upande wake Afisa wa shirika la Reli nchini TRC Catherine Mushi, amesema wananchi wanapaswa kushiriki katika kulinda miundo mbinu ya reli hiyo ikiwa ni pamoja na kuongeza uaminifu kwa wawekezaji nchini kuweza kutoa ajira zaidi kwa watanzania.