Ijumaa , 21st Oct , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Oktoba, 2016 ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa mabweni 20 ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Jiwe la msingi la mradi huo

 Mabweni hayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa Mwezi Juni mwaka huu wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho.

Wakati Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi la mradi huo, tayari ujenzi umefikia asilimia 75 ambapo majengo 20 yaliyounganishwa kimuundo yamefikia ghorofa ya nne na ujenzi huo unaofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Desemba, 2016.


Akizungumza kabla ya kuweka jiwe la msingi Rais Magufuli aliyeambatana na Mkewe Mama Janeth Magufuli ameipongeza TBA na wadau wote wanaoshiriki katika ujenzi huo zikiwemo Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa hatua kubwa ya ujenzi iliyofikiwa tangu ujenzi uanze tarehe 01 Julai, 2016 na amebainisha kuwa kwa kutumia TBA mradi huo utatumia kiasi kidogo cha fedha.

"Nawapongeza sana TBA kwa kazi nzuri mliyoifanya mpaka sasa, mradi huu utatumia Shilingi Bilioni 10 tu, Wakandarasi kutoka nje walitaka kujenga mabweni haya ya wanafunzi kwa Shilingi Bilioni 100, sasa mtaona wenyewe tumeokoa Shilingi ngapi" amesema Rais Magufuli.
 

 

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekaza Mukandala amesema wakati ujenzi huo ukiendelea chuo kimetenga Shilingi Bilioni 4.5 kutoka kwenye mapato yake kwa ajili ya kununua samani ikiwa ni pamoja na vitanda vya wanafunzi na pia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itashughulikia ujenzi wa uzio, jiko na bwalo la chakula.

Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Wabunge, Makatibu Wakuu na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda.

 

Muonekano wa Hostel hizo zitakapokamilika