Jumanne , 1st Apr , 2025

Iran imesema haitakuwa na njia nyingine ila kutumia silaha za nyuklia endapo itashambuliwa na Marekani au washirika wake.

Iran imesema hayo  kufutia kitisho cha rais wa Marekani Donald Trump aliyesema ataishambulia Iran kijeshi.
Ali Larijani, Mshauri wa kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, amesema kwenye mahojiano na televisheni ya taifa la Iran kwamba hawaelekei kwenye kuunda silaha za nyuklia, lakini ikiwa Marekani itafanya makosa katika swala hilo basi Iran italazimika kuelekea kwenye mkondo huo kwa sababu inapaswa kujilinda.

Kauli hii ameitoa saa chache baada ya kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei, kuahidi kuijibu Marekani endapo Trump atatimiza tishio lake la kulishambulia taifa hilo la Kiislamu.

Larijani amesisitiza kauli hiyo ya Kiongozi Mkuu kwamba Iran italazimika kuchukua hatua tofauti iwapo  Marekani itaishambulia nchi yake kwa mabomu au kupitia kwa Israel.

Katika mahojiano siku ya Jumamosi, Trump alisema yatafanyika mashambulizi ya mabomu ikiwa Iran haitakubali kufikia makubaliano mapya ya nyuklia. Trump pia alitishia kuiadhibu Iran kwa kuiwekea vikwazo vya ushuru
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baqaei, amesema kupitia chapisho kwenye mtandao wa X, kwamba tishio hilo linaashiria kudharau amani na usalama wa kimataifa, ambalo ni jambo la kushangaza.

Tangu aingie madarakani mwezi Januari, Trump amerejesha sera yake ya kushinikiza, ambayo katika muhula wake wa kwanza aliiondoa Marekani kutoka kwenye makubaliano ya kihistoria kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na akaiwekea tena vikwazo nchi hiyo.