Jumatatu , 24th Apr , 2023

Ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi umetajwa kuwa na faida lukuki kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani pamoja na nchi zinazotuzunguka.

Muonekano wa daraja la JPM

Miongoni mwa faida hizo ni kufupisha safari na kuokoa muda mrefu wakati wa safari hususani safari za kutoka Mwanza kwenda Geita hadi Sengerema karibu kilometa 210 ambapo kwa safari hiyo ukipitia daraja la Kigongo-Busisi ni karibu kilometa 90.

Hayo yamesemwa wilayani Sengerema na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila, akiongea na waandishi wa habari ambapo amesema ujenzi wa daraja hilo unakwenda vizuri na umefika asilimia 72.

"Daraja la Kigongo-Busisi lina umuhimu mkubwa, kwanza ni kuokoa muda, watu wanatumia masaa mwili hadi manne kwenda sehemu ya pili kwa ajili ya kuvuka lakini daraja litakapokamilika tutakuwa tunatumia dakika 4 tu kuvuka" amesema Mhandisi Mativila 

Vilevile amesema daraja hilo litakuwa kiungo muhimu kati ya mkoa wa Mwanza na mikoa jirani pamoja na nchi jirani.

"Daraja la Kigongo-Busisi linaunganisha watu wa Mwanza na mikoa ya Geita, Kagera na nchi jirani ikiwemo Uganda, daraja hili ni la muhimu sana" alisisitiza Mhandisi Mativila

Ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi ulianza mwezi Februari Februari mwaka 2020 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika tarehe 25 Februari, 2024 na unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 716 ambapo hadi sasa mradi wa ujenzi wa daraja hilo umetoa fursa za ajira zipatazo 1,001.