Alhamisi , 25th Sep , 2014

Mwenyekiti wa Taasisi ya sekta binafsi nchini Tanzania TPSF, Dk. Reginald Mengi leo amewataka wanawake nchini Tanzania kujitambua na kuondokana na dhana ya kuwa kazi za uchimbaji madini ni kazi za wanaume pekee.

Mwenyekiti Taasisi ya Sekta Binafsi nchini Tanzania (TPSF), Dkt Reginald Mengi.

Kwa mujibu wa Dkt Mengi, kuachana na fikra hiyo kutawawezesha wanawake kujijengea uwezo wa kujitegemea kwa kujihusisha na uendelezaji wa rasilimali zilizopo.

Dkt Mengi ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akifunga mkutano mkuu wa siku mbili wa chama cha wanawake wachimbaji madini Tanzania (CHAWOMA) na kuainisha kuwa wanawake wanaojishughulisha na uchimbaji madini ni mashujaa kwani wamefahamu fursa itakayowaondolea umaskini.

Dk Mengi amesema wanawake wanatakiwa kutambua kuwa Tanzania sio maskini na kuwataka kuwa na macho yanayoona fursa na utajiri uliopo nchini na kuitaka serikali kuwasemehe tozo wachimbaji wadogo wadogo kwani tozo wazotozwa haziendani na nia ya serikali ya kuzalisha ajira nchini.