Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam imefuta ratiba ya kuwaona wagonjwa nyakati za mchana ili kuwaletea chakula kuanzia Julai mosi mwaka huu kutokana na kueleza kuwa wameboresha huduma za utoaji chakula katika hospitali hiyo.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma Hosptali ya Taifa Muhimbili Bw. Aminieli Eligaesha Buberwa wakati akiongelea maboresho ya utoaji wa chakula yaliofanyika katika hospitali hiyo.
Bw. Eligaesha amesema lengo la kuondoa muda wa mchana kwa ndugu wanaofika kupeleka chakula kwa wagonjwa hospitalini hapo ni kutoa fursa kwa wahudumu wa afya kuwahudumia wagonjwa kwa umakini zaidi huku akifafanua kuwa jukumu la kutoa huduma kwa wagonjwa hospitalini hapo nia la wahudumu wa afya na si la ndugu.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa na uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhusu uboreshaji wa chakula kwa wagonjwa inaruhusu mgonjwa kuagiza pia kupikiwa chakula chochote kwa makubaliano ya gharama.

