
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro
Uamuzi huo wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuingia mtaani kusaka wahalifu hao, ni kufuatia kuripotiwa kwa matukio kadhaa ya uvamizi usiku unaodaiwa kufanyika na 'Panya Road' katika maeneo ya Bunju wakitumia silaha mbalimbali zikiwemo mapanga, visu na mashoka.
Akizungumza Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema, "Tusilaumiane malengo ya Jeshi la Polisi ni kuwakamata watuhumiwa, kukamilisha uchunguzi, na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, lakini wakijitoa ufahamu wakajaribu kushambulia Polisi watajihami kwa kutumia nguvu inayolingana na mashambulizi na aina ya silaha wanazozitumia,".
Wakizungumza baadhi ya wananchi waliovamiwa na panya road hao wamesema kwamba walimning'iniza mtoto mdogo na kutishia watamkata mapanga endapo mzazi wake angeshindwa kutoa simu, laptop na fedha zote alizonazo, na kwamba walifanikiwa kuchukua vitu hivyo na kumuacha mtoto salama.
"Walivyoingia ndani hawakutaka kuuliza wakaanza na mama wakaanza kumpiga wanataka simu, wakaingia chumbani wakamchukua mtoto na kumning'iniza juu wakamwekea panga wakasema kama unampenda mtoto wako tupe kila kitu simu na hela, baadaye wakamtaka dada yangu avue nguo wambake, alivyokataa wakaanza kumpiga, lakini waliondoka," amesema Brightness.