Jumamosi , 18th Apr , 2015

Makundi ya vijana nchini wanatarajiwa kunufaika na fursa za ajira kupitia mfumo mpya wa teknolojia ya simu za mkononi, unaomtaka kijana kujiunga kwenye mtandao na kumuunganisha mwingine, ili kuweza kuzalisha kipato cha ziada na kukuza uchumi.

Huduma za Simu ya mkononi kuwakomboa vijana Tanzania.

Mfumo huo pia,unatarajiwa kuwaunganisha vijana pamoja kwa kuunda mtandao utakaowaingiza katika ajira ya moja kwa moja na kuondoa changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira iliyopo hapa nchini.

Mkurugenzi wa kampuni ya Rifaro Afrika mkoani Arusha, inayaunganisha vijana kupitia mfumo huo Immaculate Mkodo, amesema lengo ni kufanikisha mpango wa kutoa ajira kwa vijana kupitia mawasiliano ya simu za mkononi.

Akizungumza jijini Arusha katika zoezi la utoaji elimu kuhusu mfumo huo, Immaculate amesema mfumo huo utamwezesha kijana kupatiwa muda wa maongezi wa shilingi elfu kumi kwa mwezi, ambapo kupitia muda huo mhusika atakuwa akilipwa kiasi cha fedha kulingana na matumizii yake.

Mwenyekiti wa bodi ya ushauri ya RIFARO Africa, Amenye Mwakisambwe amesema mfumo huo utawasaidia sana vijana kujipatia kipato kwa kutumia vizuri fursa za teknolojia ya mawasiliano huku baadhi ya vijana walio katika mpango huo wakibainisha kuanzisha miradi binafsi ya ujasiriamali ambayo imewasaidia kuondokana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

Pamoja na uwepo wa fursa hiyo ya kujipatia kipato kupitia teknolojia ya mawasiliano, changamoto imetolewa pia kwa watanzania kuwa na uelewa juu ya masuala ya hisa ili kwenda sambamba na maendeleo ya kiuchumi duniani.