Ijumaa , 16th Jan , 2015

Mamlaka ya udhibiti wa safari za majini na nchi kavu (Sumatra) imebaini kuwepo kwa bandari bubu 45 katika wilaya za Mkinga, Tanga na Pangani ambazo zimekuwa zikipitisha abiria na bidhaa za magendo.

Mamlaka ya udhibiti wa safari za majini na nchi kavu (Sumatra) imebaini kuwepo kwa bandari bubu 45 katika wilaya za Mkinga, Tanga na Pangani ambazo zimekuwa zikipitisha abiria na bidhaa za magendo kufuatia baadhi ya vyombo vya majini ikiwemo boti na mtumbwi kubainika kutumika kwa ajili ya kubeba abiria ambao wengi wao ni wafanyabiashara kutoka kisiwani Zanzibar.

Akizungumza na EATV baada ya ukaguzi uliofanywa katika wilaya tatu za mkoa wa Tanga kubaini kuwepo kwa bandari hizo ambazo zimekuwa zikiikosesha serikali mapato yake ya msingi afisa mdhibiti mkuu wa Sumatra wa Tanga Bwana Walukani Luhamba ameagiza wamiliki wa vyombo hivyo kuacha mara moja shughuli za kusafirisha abiria bila kufuata taratibu zinazokubalika.

Ametoa mfano kuwa wilaya ya Pangani kati ya tatu zilizofanyiwa utafiti imebainika kuwa ndiyo inayoongoza kwa kufanya shughuli hizo ambazo hazijafuata vigezo vya kisheria kwa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na Tanzania bara ikiwa ni pamoja na kufanyiwa ukaguzi kabla ya kubeba bidhaa za wafanyabiashara na abiria hatua ambayo inahatarisha maisha ya watu.

Hata hivyo baadhi ya abiria waliokutwa na EATV katika bandari bubu ya Kasera ambapo wavuvi pia hutumia sehemu hiyo kuwa ndio soko kuu la kuuza samaki wameiomba serikali kuwaruhusu wafanyabishara kutumia vyombo vyao kwa ajili ya kubeba abiria kwa sababu kuna idadi kubwa ya abiria kila siku wanaokwenda kisiwani Pemba.