Jumatano , 22nd Feb , 2017

Mbunge wa jimbo la Chalinze Mhe. Ridhiwan Kikwete amefunguka mapya juu ya yeye kuhusishwa na dawa za kulevya na kusema yeye hajawahi kufanya biashara hiyo na kudai ni bora yeye kufa masikini kuliko kkutafuta utajiri kwa njia ya dawa za kulevya

Ridhiwan Kikwete

Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema hayo kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa kiongozi huyo anafanyiwa uchunguzi ili serikali ijiridhishe na tetesi hizo zilizopo mtaani kuwa anafanya biashara ya dawa za kulevya.

Kiongozi huyo kupitia mitandao yake ya kijamii ameshukuru kusikia taarifa hiyo na kusema huenda uchunguzi huo ukaleta faraja kwake na unaweza kuleta ukombozi na kuweza kuzima uvumi huo ambao unaonesha yeye mwenyewe unamtesa na kumkera. 

"Ni jambo jema na la faraja kubwa kwangu kama uchunguzi unafanywa. Ni ukombozi kwangu, naamini ukweli utajulikana kuwa ni uvumi tu usiokuwa na chembe ya ukweli. Ni maneno ya watu wasionitakia mema. Sina la kuficha sifanyi biashara hiyo haramu na wala sijawahi kufikiria kufanya. Ni bora kufa maskini kuliko kutafuta utajiri kwa njia hiyo" alisisitiza Mhe. Ridhiwan Kikwete.