Serikali yatoa miezi sita

Wednesday , 11th Oct , 2017

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa miezi sita kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari nchini kuanzisha madawati ya ulinzi na usalama wa watoto kwa ajili ya kusikiliza matatizo ya wanafunzi.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike kitaifa iliyofanyika Wilaya ya Tarime Mkoani Mara amewasisitiza wakuu wa shule za msingi na sekondari kuzingatia uwepo wa dawati la ulinzi na usalama wa mtoto kike katika shule zao ili kuwa salama na kuwa na mahali pa kueleza matatizo yao.

Mh. Ummy ameongeza kuwa suala la kumlinda mtoto wa kike ni jukumu la kila mmoja katika jamii na kuwapongeza wadau wa maendeleo ya watoto kwa jitihada zao na kushirikiana na serikali kutoa elimu kwa wanajamii kuhusu madhara ya mimba za utotoni, ukeketaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la kutokomeza ukeketaji Tarime Stela Mgaya amesema kuwa wamefanikisha kuwaondoa mangariba 63 kutoka katika kazi ya ungariba na kuwatafutia kazi nyingine za kujipatia kipato.