Ibada imefanyika katika Kanisa alilokuwa akisali mtangazaji huyo tangu kuzaliwa kwake mpaka umauti ulipo mkuta
Mwili wa Mtangazaji Mkongwe wa vipindi vya muziki wa Dansi Nchini Sunday Mwakanosya umeagwa leo Januari 02, katika kanisa la KKKT DMP Usharika wa Ukonga Jijini Dar es Salaam kwaajili ya kwenda kwenye maziko Kyela Jijini Mbeya baada ya kuugua ghafla Disemba 25, 2024.
Ibada imefanyika katika Kanisa alilokuwa akisali mtangazaji huyo tangu kuzaliwa kwake mpaka umauti ulipo mkuta na wananchi na waumini walioshiriki katika ibada hiyo wameaswa kuweza kuishi vyema ili kuweza kuacha alama nzuri Duniani.
"Hapa kanisani Sunday amekuwa akishiriki vyema tangu alipo zaliwa lakini hapa napenda kuwaasa kuishi vyema na kuhakikisha katika muda tuliopo hapa duniani tunatenda mema, hakuna mtu anayejua lakini tukiishi vizuri mwisho wetu utakuwa salama". Amesema Mch. Ismail Mwipile – Mchungaji wa KKKT Usharika wa Ukonga na Segerea
Wakati ukisomwa wasifu wa marehemu imeelezwa kuwa alikuwa mtangazaji aliyefanya katika chombo cha habari cha ITV na Channel 10 mpaka umauti ulipo mkuta huku akiwa ameacha mtoto mmoja.
"Sunday Mwakanosya ni baba na mtoto wa pili kati ya watoto wa 3, 200 mpka 2004 pamoja na ITV 2004 mpka 2007 na channel 10, Aliumwa Ghafla ugonjwa wa shinikizo la Damu 25, Decemba huku akiacha mtoto Mmoja wa Kike". Amesema Esther Mwakanosya, Mdogo wake marehemu.
Waandishi wa habari na watu wakaribu na marehemu wameeleza jinsi alivyokuwa na mchango mkubwa katika maisha yao na uwajibikaji wake na ushiriki katika jamii na huduma aliyokuwa akiitoa.
"Kwa sisi watu wa muziki tasnia yetu imekuwa haina tena mtu mahiri na tumepungukiwa maana alikuwa anasaidia sana muziki wetu wa dansi". Amesema Rajabu Zomboko, Mtangazaji wa Radio one na ITV.
"Sunday ameondoka huku akituachia pengo kubwa sana na mpaka sasahivi hatujui nani anaweza kukaa nafasi yake, kama sikuile tu tumepata tairifa ya kuumwa kwakwe ilikua tabu sana kupatikana mbadala wake". Amesema Salumu Mkambala, Mtangazi Chanel Ten.
"Hapa hatuna namna wala lakusema ila kiukweli inasikitisha sana kwakuwa mmoja wetu hapa amesha ondoka na bado tulikuwa tunamuhitaji". Amesema Cecy Nwasikitoko, Mtangazaji Uhuru FM.
"Mimi alikuwa akinisihi kuoa kila muda na siku si nyingi yeye ndiye aliyesimamia na kupambania harusi yangu sasa niliposikia amefariki nimepata shida kidogo". Amesema Fredrick Ukani Bogoss, Mwanamuziki wa Dansi chini ya Nyoshi El Saadat.
"Nilikuwa napenda sana kufuatilia muziki wa Dansi na nilikuwa mpaka na namba yake nilikuwa nampigia namsauri na ananisikiliza". Amesema Saburi Mzinga, Mfuatiliaji na Mpenzi wa Mziki wa Dansi.
Mwili wa Sunday Mwakanosya umesafirishwa leo kuelekea Kyela Jijini Mbeya kwaajili ya maziko baada ya umauti kumkuta katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Disemba 30, 2024 alipokuwa akipatiwa matibabu.