Jumanne , 23rd Dec , 2025

“Habari hiyo haikuripotiwa kwa wakati katika kituo chochote cha Polisi kabla ya kupelewa jana Disemba 22 na shemeji yake aitwaye Kelvin Leonard majira ya saa 12:00 jioni,” taarifa ya polisi imeeleza.

Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani limekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Instagram ikieleza kuhusu gari la Jeshi la Polisi kumgonga mwananchi eneo la Kongowe wilayani kibaha na kusababisha kifo chake.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani iliyotolewa leo Disemba 23,2025 imeeleza kuwa, Disemba 19 majira ya saa 2:00 usiku katika eneo hilo la Kongowe katika Barabara ya Morogoro Dar es Salaam, gari ambalo halikutambulika namba za usajili likitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam lilimgonga mwanamke aliyetambulika kwa jina la Pendo Mugisa Mashauri (20), mkulima mkazi wa Kongowe na kumsababishia majeruhi.

“Habari hiyo haikuripotiwa kwa wakati katika kituo chochote cha Polisi kabla ya kupelewa jana Disemba 22 na shemeji yake aitwaye Kelvin Leonard majira ya saa 12:00 jioni,” taarifa ya polisi imeeleza.

Imeelezwa kuwa, mara baada ya ajali hiyo, wananchi walimkimbiza majeruhi katika kituo cha afya cha White Hope kilichopo Miembesaba, Kibaha ambapo alipatiwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa matibabu zaidi.

“Tarehe 20 Disemba, 2025 majira ya saa 9:00 usiku alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo”, taarifa hiyo imeongeza.

Taarifa ya polisi imesema hakuna shuhuda anayethibitisha kutambua aina ya gari ambalo lilimgonga Pendo Mugisa Mashauri hivyo msako mkali unaendelea kubaini gari lililosababisha ajali hiyo. Jeshi la Polisi limewataka wananchi kupuuza taarifa zinazosambazwa pasi na uthibitisho wa mamlaka husika.