Jumatano , 7th Dec , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Desemba, 2016 amefanya uteuzi wa Katibu Mkuu mmoja na Mkuu wa Mkoa mmoja na pia amefanya mabadiliko madogo katika Wizara na Mikoa kama ifuatavyo;

Christopher Ole Sendeka

Amemteua Bw. Christopher Ole Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe akichukua nafasi ya Dkt. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

Dkt. Rehema Nchimbi anajaza nafasi iliyoachwa na Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo anayeshughulikia Kilimo nafasi ya Dkt. Frolence Turuka ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Dkt. Turuka  anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Job Masima ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Dkt. Osward J. Mashindano kuwa Msajili wa Hazina akichukua nafasi ya Bw. Lawrence Mafuru ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Lawrence Mafuru

Dkt. Magufuli amemteua Prof. Faustin Kamuzora kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais. Kabla ya uteuzi huo, Prof. Kamuzora alikuwa Katibu Mkuu Mawasiliano.

Rais Magufuli pia amemteua Dkt. Maria Sasabo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na atakuwa akishughulikia Mawasiliano kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Prof. Faustin Kamuzora.

Pia Rais Magufuli amemteua Mhandisi Angelina Madete kuwa Naibu Katibu Mkuu Katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. Maria Sasabo aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano.

Aidha, Rais Magufuli amemteua Dkt. Aloyce K. Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Dkt. Osward Mashindano - Msajili wa Hazina (Mteule)