Jumatano , 29th Jun , 2016

Tanzania inakabiliwa na nguvukazi inayohitajika katika uzalishaji, kutokana na elimu inayotolewa na vyuo mbali mbali nchini, kutoendana na mahitaji halisi ya sekta binafsi na hivyo kuwa moja ya changamoto kuelekea kuwa nchi ya uchumi wa kati.

Baadhi ya washiriki wa warsha ya siku moja iliyokuwa inaangalia ukosefu wa nguvu kazi katika uchumi. Katikati ni balozi wa Ufaransa nchini Bi. Malika Berak.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo na washiriki wa warsha ya siku moja iliyoandaliwa na serikali ya Ufaransa kupitia ubalozi wake hapa nchini, warsha iliyokuwa inaangalia ukosefu wa nguvu kazi katika uchumi kulingana na uzoefu wa sekta binafsi hapa nchini.

"Kwa muda mrefu kumekuwa hakuna uwiano kati ya nguvukazi inayohitajika katika uzalishaji na taaluma waliyonayo wahitimu wa vyuo mbali mbali nchini...hii imekuwa na athari kubwa kwa uchumi kwani mwisho wa siku watu wanaoajiriwa na sekta binafsi wanakosa sifa za kuwa wafanyakazi wazuri," amesema mwakilishi wa sekta binafsi Bw. Isack Kiwango.

Bw. Kiwango amesema kuna umuhimu wa kuhuisha mitaala ya masomo ili elimu inayotolewa iwe inaakisi mahitaji ya sekta binafsi na hili linawezekana kwa pande mbili hizi kukutana na kuona ni kwa namna gani mitaala hiyo inaweza kubadilika.

Kongamano hilo lilihudhuriwa pia na washiriki kutoka taasisi za elimu ya juu nchini ambapo mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Profesa Prosper Ngowi amezungumzia ukosefu wa sehemu za mafunzo ya kazi kwa vitendo na hatua zinazochukuliwa na chuo hicho katika kukabiliana na hali hiyo.

"Ni kweli kuna changamoto ya ukosefu wa mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wengi wa elimu ya juu, sisi kama wakufunzi tunaichukulia hii kama changamoto ya kuona ni kwa namna gani tunaandaa vijana wetu ili waje kuwa nyenzo nzuri katika uzalisha," amesema Profesa Ngowi.

Ameongeza kwa upande wa Chuo Kikuu cha Mzumbe wameiona changamoto hiyo na tayari kama chuo kimeshaanza kuchukua hatua ya kuandaa madodoso yanayopelekwa kwa waajiri ambao baadaye hutoa maoni yao ni kwa namna gani wanafunzi wanapaswa kuandaliwa ili kukidhi mahitaji ya sekta binafsi.

"Hata hivyo changamoto nyingine ni ufinyu au kutokwepo kwa utayari wa sekta binafsi kupokea wanafunzi wanaoomba field attachment au hata internship, nadhani hii ni changamoto kwa sekta binafsi nayo ijiangalie ni kwa namna gani itakuwa tayari kutoa fursa ya mafunzo kwa vitendo,".

Kwa upande wake, Balozi wa Ufaransa hapa nchini Bi. Malika Berak amesema ukosefu wa rasilimali watu ni moja ya changamoto inayoyakabili mataifa mengi duniani ambapo ameishauri serikali kuweka mkazo katika elimu kama njia ya kupunguza ukosefu wa nguvu kazi katika uzalishaji.