Jumanne , 21st Jun , 2016

Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amehimiza wanawake wajasiriamali wa Tanzania Bara na Visiwani kujiunga na majukwaa ya kuwezesha wanawake kiuchumi yatakayoanzishwa kote nchini kwa ajili ya kupata elimu ya ujasiriamali.

Mheshimiwa Samia alitoa rai hiyo leo wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wanawake wajasiriamali yaliyoandaliwa na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) katika Bwalo la JKT Mgulani, Dar es salaam.

Alisema kama wanawake watayatumia majukwaa hayo ya kiuchumi watakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa bora, kutafuta masoko, kupanga bei nzuri za bidhaa na kupata fursa za mikopo.

Aidha, Makamu wa Rais aliwasihi wanawake wajasiriamali kuichukulia ajira hiyo kama ajira yo yote rasmi kwa kuwa serikali itaweza tu kutimiza azma yake ya kupunguza ukosefu wa ajira kupitia sekta ya viwanda vidogo vidogo ambavyo vingi vinaendeshwa na wajasiriamali.

“Kupitia majukwaa niliyoyataja ya kumwezesha mwanamke kiuchumi nitajihidi kuhakikisha kuwa majukwaa haya yanatoa majibu ya changamoto zinazowakabili wanawake wajasiriamli na kuchangia ukuaji wa ajira, kuondoa umaskini na kuwezesha ujenzi wa Taifa la viwanda,” alisema

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa EOTF Mke wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mama Anna Mkapa alisema tangu Mfuko huo uanzishwe miaka 19 iliyopita umetoa mafunzo kwa zaidi ya wanawake wajasiriamali 30,000 na umewezesha wajasiriamali 14,500 kushiriki maonesho ya sabasaba ili kutangaza na kuuza bidhaa zao.

“Wanawake hawa wamejenga nyumba bora, kusomesha watoto, kulipia huduma za matibabu, shughuli za kifamilia kutokana na mafanikio ya biashara zao zilizoborehwa na mafunzo hayo.

Mama Mkapa alimwahidi Makamu wa Rais kuwa mfuko huo utaendelea na jitihada zake za kutoa elimu kwa wanawake wajasiriamali na kuwawezesha kushiriki katika maonesho ya biashara.

Katika mafunzo hayo wanawake wajasiriamali wataelimishwa jinsi ya kupata mitaji na matumizi ya mashine za EFD; magonjwa hatarishi kama vile ukimwi, saratani na malaria pamoja na suala zima la mirathi na ujasiriamali kwa ujumla.