Jumamosi , 26th Nov , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, ametunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi 194 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  kundi la 59/15 katika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akikagua gwaride la heshima linaloundwa na Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kabla hajawatunuku kamisheni katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam Novemba 26, 2016

Hii ni mara ya kwanza kwa Maafisa Wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni nje ya Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kilichopo mkoani Arusha, na ni mara ya kwanza kwa Maafisa Wanafunzi wa JWTZ kutunukiwa Kamisheni ndani ya  Ikulu  tangu chuo hicho kihamishiwe Monduli mkoani Arusha kutoka Jijini Dar es Salaam mwaka 1976.

Maafisa hao ambao 168 ni wanaume na 26 ni wanawake, wametunukiwa Kamisheni katika cheo cha Luteni Usu na sasa wamekuwa Maafisa Wapya wa JWTZ.

Kabla ya kutunuku Kamisheni, Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa na Maafisa wanafunzi wa JWTZ na baadaye akashuhudia uhodari wa askari kutoka kikosi cha maadhimisho cha JWTZ waliofanya onesho la gwaride la kimyakimya.

Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akitunuku kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam  Novemba 26, 2016

Akitoa taarifa fupi ya mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo hicho Meja Jenerali Paul Peter Masao amesema katika mafunzo hayo, jumla ya wanafunzi 221 ndiyo walioanza, lakini waliohitimu ni 194, huku wengine 27 wakishindwa kuhitimu kwa sababu mbalimbali.

Pia amesema mmoja kati ya 194 waliotunukiwa kamisheni hizo leo, alipatia mafunzo yake nchini Uingereza ambapo kwa mujibu wa utaratibu, anapaswa kuungana na wenzake nchini kwa ajili ya zoezi hili mbele ya Amiri Jeshi Mkuu.

Akizungumza baada ya chakula cha mchana katika ukumbi wa Ikulu Rais Magufuli amesema Serikali itahakikisha inaboresha zaidi maslai na mazingira ya kazi kwa Jeshi hilo na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiongea baada ya kutunuku  kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) katika ukumbi wa mikutano wa Ikulu jijini Dar es salaam  Novemba 26, 2016

Aidha, Rais Magufuli amesema ameamua tukio hili la kutunuku Kamisheni lifanyike Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutoa heshima kwa Maafisa wa JWTZ kama ambavyo Viongozi wengine Serikalini wamekuwa wakipata heshima ya kuapishiwa Ikulu.

"Kwamba Mawaziri tunapotaka kuwaapisha tunawaapishia hapa, Wakuu wa Mikoa tunawaapishia hapahapa, Makatibu Wakuu tunawaapishia hapahapa, kwa nini hawa Maafisa wa Jeshi tusiwaapishie hapahapa kwenye nyumba yao? Nyinyi ndio mnalinda nchi, nyinyi ndio mnasimamia usalama wa nchi hii, lakini nikiuliza hapa inawezekana wengine mpaka wamekuwa Mabrigedia Jenerali hawajawahi kukanyaga Ikulu, wakati hapa ni kwenu" amesema Rais Magufuli.

Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiweka saini kwenye hati  ya  kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wa Kundi la 59/15 wa Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) kabla hajawatunuku katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es salaam leo Novemba 26, 2016

 

Sherehe za kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi hao zimehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi na Wakuu wa Jeshi la Ulinzi wastaafu na Majenerali wastaafu wa JWTZ.