Ijumaa , 25th Nov , 2016

Sababu ya asilimia kubwa ya watoto duniani kuzaliwa wakiwa na matatizo ya moyo bado haijabainika hivyo suala la watoto kupimwa ugonjwa wa moyo wakiwa bado tumboni ni muhimu ili kupunguza idadi yao wanaopoteza maisha kwa kukosa matibabu ya matibabu

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete-JKCI iliyopo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili  Dkt Bashiri Nyangasa amesema kuwa katika kipindi cha muda wa wiki moja taasisi hiyo imefanya jumla ya oparesheni 17 za upasuaji wa moyo na kifua ambapo kati ya hizo watoto ni 12 na watu wazima ni 5 hali inayoonesha kiwango cha watoto wenye matatizo ya moyo kuwa kikubwa nchini.

Amesema kuwa oparesheni hizo zimefanyika kwa utaalamu mkubwa kwa ushirikiano wa madaktari bingwa wa moyo kutoka Tanzania pamoja na madaktari bingwa wa moyo kutoka Australia ambapo wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji mpaka sasa wapo katika hali salama.

Naye Daktari Bingwa wa upasuaji moyo watoto  kutoka taasisi hiyo Dkt. Godwini Godfrey amebainisha kuwa mwaka jana katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete walizaliwa watoto zaidi ya elfu kumi na tano wenye matatizo ya moyo na kuongeza kuwa kwa mwaka huu wamefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo na kifua kwa wagonjwa 345 ambao ni watu wazima na watoto huku idadi kubwa ya watanzania ikiendelea kusubiri kupata matibabu ya magonjwa ya moyo na kifua.