Jumatatu , 11th Oct , 2021

Rais Samia Suluhu Hassan ameonya viongozi wanaosambaza sumu ya ukabila baada ya kuwajibishwa wanapokuwa wameharibu kwenye majukumu yao huku akisisitiza yeye haangalii kabila kwenye kuteua mtu.

Rais Samia Suluhu Hassan

Ameyasema hayo leo Oktoba 11, 2021 Ikulu Chamwino Dodoma, wakati akiongea baada ya kuwaapisha viongozi wateule, Mhe. Sophia Edward Mjema, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Jaji Omar Othman Makungu, kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania na Mhe. Jaji Mustapha Siyani, kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

''Watu wanafanya makosa ukiwashika ukiwawajibisha, nimewajibishwa kwa sababu ni wa kabila fulani, sina kabila mimi ukiniuliza kabila langu nani nitakwambia ni Mzanzibari. Hiyo sumu mnaipeleka sana na naomba isimame. Mwalimu Nyerere alitufundisha kufanya kazi bila kuangalia makabila,'' ameeleza Rais Samia Suluhu.

Aidha, amesisitiza kuwa, ''Mimi siangalii kabila, TAMISEMI kwa mfano Waziri ni Mtanga, Katibu Mkuu Mtanga na wengine, nikaletewa hapa mama umeweka wote watanga, nikauliza wana sifa? waacheni wafanye kazi wakikoroga nawatumbua, sipangi kwa makabila napanga kwa uwezo twende tukasukume maendeleo ya wananchi''.

Tazama Video hapo chini