Jumanne , 12th Dec , 2017

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka watanzania kukemea vitendo vinavyodhihirisha mmomonyoko wa maadili, ikiwemo mabinti wanaocheza utupu kwenye video za muziki.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye mkutano wa Jumuiya ya Wazazi mjini Dodoma, na kusema kwamba huwa anashangazwa kila anapowasha Television kutazama muziki, na kukutana na mabinti wakicheza utupu huku wanaume wakiwa na mavazi ya staha, na kusema kwamba ni aibu kubwa kwa wazazi kuangalia mambo hayo.

“Mimi ni shabiki mzuri wa muziki, kila ukifungulia mziki wanaocheza utupu ni wanawake wanaume hapana., nyinyi kama jumuiya ya wazazi umefika wakati wa kukemea mambo haya, tunawafundisha nini watoto wetu, tunapenda mziki, lakini je, hiyo ndio muziki tunayocheza, tumeingiliwa na mdudu gani, saa nyingine unapoangalia TV na watoto wetu ni aibu kubwa, yanayofanyika pale ni aibu, si kwa sababu sitaki watu wastarehe, kama ni kwenye klabu kavue huko, lakini kwa nini uwavulie hata wasiohitaji kuona uc**? Tena kwa muda usio muafaka?”, amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameendelea kwa kuitaka jumuiya hiyo na watu wote kusimamia maadili, huku akivinyooshea mkono vyombo husika vinavyopaswa kushughulika na masuala ya utamaduni wa Mtanzania.

“Ifike mahali sisi kama watanzania, bila kujali vyama vyetu, tulinde maadili yetu, ninyi kama wazazi, sifahamu kama enzi za akina Fatma Karume au kina Maria Nyerere huo ndio ulikuwa mtindo, lakini nina uhakika enzi zile haikuwa hivyo, lakini vyombo vyetu vya habari, wasimamizi wa maadili haya wako wapi, wizara inayosimamia haya wako wapi, je, TCRA wako wapi, Niwaombe ndugu zangu Jumuiya ya wazazi kuikosoa hata serikali kwenye kusimamia maadili ya Tanzania”, amesema Rais Magufuli.