Ijumaa , 23rd Oct , 2020

Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi, (CCM), Dkt. John Magufuli, amesema kuwa anawashangaa watu wanaopanda majukwaani na kusema kuwa yeye hampendi aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, na ndiyo maana alimfukuza kazi hiyo.

Kushoto ni mgombea urais kupitia CCM Dkt John Magufuli na kulia ni mgombea ubunge wa jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo.

Magufuli ametoa kauli hiyo hii leo Oktoba 23, 2020, akiwa mkoani Arusha akiendelea na mikutano yake ya kampeni wakati akiwaomba wana Arusha wamchague yeye, Mbunge pamoja na madiwani kutoka CCM kwani hataki kuchanganyiwa.

"Nataka niwaambie Gambo sikumfukuza u-RC wala aliyekuwa DC hapa, na bahati nzuri Gambo aliniomba, akaniambia mzee nimeiona Arusha inaenda vibaya ninaomba nikaikomboe nikawe mbunge wa Arusha, nikamuambia nenda na Mungu akusaidie, sasa ninawashangaa wanaosema Gambo simpendi", amesema Magufuli.

Aidha Magufuli ameongeza kuwa, "Ningekuwa simpendi nisingerudisha jina lake kuja kugombea, wana Arusha mkitaka maendeleo na mabadiliko ya kweli nileteeni Gambo, nitashangaa sana kama malipo yenu kwa mtu aliyewatetea itakuawa kumnyima kura, Gambo nimemsumbua mambo mengi".