Jumamosi , 28th Sep , 2024

Mwili wa Askari namba NV 1630 SGT HAJI Machano Mohamedi wa kikosi cha Valantia (KVZ) Makao Makuu Mtoni Zanzibar aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha umeokotwa kwenye msitu uliopo karibu na kambi ya chuo hicho ukiwa umeharibika vibaya

Taarifa ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kusini Unguja SACP Daniel E. Shillah imeeleza kuwa Askari huyo alikuwa akihudhuria mafunzo ya Uongozi ( officer cadet) katika Chuo cha Uongozi cha Jeshi La Kujenga Uchumi Dunga. 

Imeelezwa kuwa Tarehe 08/08/2024 majira ya saa 8:00 mchana katika msitu uliopo karibu na chuo hicho. Askari huyo akiwa na wenzake katika mafunzo alipotea katika mazingira ambayo hayakueleweka, baada ya wenzake kurejea kambini ndipo ilipo bainika kwamba askari huyo alikuwa haonekani ndipo taarifa hizo zilipelekwa Polisi kituo cha Dunga na uchunguzi kuendelea.

"Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Afisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ulibaini mwili huo ukiwa na nguo na viatu ambazo zinafanana na zile alizovaa askari huyo siku aliyopotea"

"Aidha, katika mfuko wa suruali aliyokuwa amevaa ilipatikana simu ambayo imetambulika kuwa ni ya kwake aliyokuwa akiitumia" imeeleza taarifa hiyo ya Polisi

Polisi wamesema kuwa uchunguzi zaidi wa tukio hilo unaendelea ukiwepo ulinganisho wa vinasaba (DNA) kwa madhumuni ya kubaini ni kitu gani kilicho mkuta na kupoteza uhai ili hatua nyingine za kisheria zifuate.