Jumatatu , 29th Dec , 2014

Waziri wa uchukuzi Mh. Dk. Harrison Mwakyembe ametoa muda wa miezi 11 kwa mkandarasi wa mradi wa ujenzi wa ghati la meli katika kisiwa cha kome wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza unaotarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.

Waziri wa uchukuzi Mh. Dk. Harrison Mwakyembe

Mradi huo uliopo katika kijiji cha Ntama, jimbo la Buchosa wilayani Sengerema unajengwa na mkandarasi kampuni ya Gemen Engineering baada ya mamlaka ya bandari Tanzania kutenga shilingi bilioni mbili.

Waziri wa uchukuzi Mh. Dk. Harrison Mwakyembe ametembelea mradi huo na kumuagiza mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo mhandisi Andrew Nyantori kuhakikisha anaukamilisha kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika.

Akiongea katika mkutano wa hadhara baada ya waziri kutembelea mradi huo, mbunge wa jimbo la Buchosa ambaye pia ni naibu waziri wa uchukuzi Mh. Dk. Charles Tizeba amesema wananchi wamekuwa wakihangaika kupata usafiri wa meli za kwenda Mwanza kutokana na kisiwa hicho cha kome kutokuwa na ghati la meli kutia nanga.

Pia mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Gemen Engineering mhandisi Andrew Nyantori pamoja na mkuu wa bandari ya Mwanza Patrick Namahuta wameelezea jinsi mradi huo utakavyotekelezwa.