Jumatatu , 19th Feb , 2018

Familia mbili za wanandoa Baraka Malali na Ashura Mussa waliokamatwa nchini China Januari 19,2018 wakiwa na mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili zimekubaliana mtoto atunzwe na babu yake Hashim Mbarouk.

Hayo yamebainishwa na Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii, Daniel Masunzu leo wakati wakizungumza na wanahabari ambapo amesema kwamba Mbarouk ni babu upande wa mama aliyempokea mtoto huyo aliporejeshwa nchini Februari 14,2018.

Masunzu amesema baada ya majadiliano na pande hizo mbili, amesema muafaka umepatikana mtoto atakuwa chini ya familia ya Mbarouk na Zuhura Nyangasa ambaye ni bibi yake upande wa mama.

Familia zote mbili zimekubaliana kuhusu hatua hii. Mtoto kukaa upande wa Mbarouk haina maana kwamba matunzo watayatoa wao peke yao, bali ndugu wengine wana jukumu la kuendelea kufanya mawasiliano na mtoto kwa ajili ya matunzo,” amesema Masunzu.

Wanandoa hao (Baraka na Ashura ) walikamatwa China Januari 19,2018 wakiwa na mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili na miezi tisa wakituhumiwa kupatikana na dawa za kulevya.