Ijumaa , 27th Jul , 2018

Mtu aliyethibitika kuwa na umri mkubwa zaidi duniani amefariki akiwa na umri wa miaka 117 na siku 81 kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa leo na wizara ya Afya nchini Japan.

Bi. Chiyo Miyako enzi za uhai wake.

Chiyo Miyako ambaye alikuwa raia wa Japan alifariki Jumapili iliyopita alipokuwa amelazwa hospitalini ingawa ugonjwa uliokuwa unamkabili haukuwekwa wazi.

Miyako alithibitishwa kuingia kwenye rekodi ya kitabu cha rekodi ya dunia cha Guinness, akitajwa kuwa mtu mwenye umri mkubwa zaidi duniani anayeishi na pia mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi duniani aliyeishi.

Kwa mujibu wa rekodi, Miyako alizaliwa Mei 22 mwaka 1901 katika mkoa wa Kansai, eneo la Wakayama nchini Japan. Familia yake imemuelezea kama mwanamke aliyekuwa mcheshi na wa pekee wakati wa maisha yake. Wameeleza kuwa moja kati ya sifa yake kuu ilikuwa uvumilivu.

Familia hiyo imesema kuwa enzi za uhai wake alikuwa anapenda kula vyakula vya Kijapan aina ya ‘shush na eel’,( chakula cha kijapani chenye Mchanganyiko wa Majani na Samaki)  alipenda kufanya mazoezi ya kupiga picha, kunywa Mvinyo na kuvuta sigara kwa muda mrefu.

kwa mujibu wa kitabu cha dunia cha kuweka rekodi cha Guinness Mtu aliyebakia mwenye umri mkubwa nchini Japan ni mwanaume mzee aitwaye Masazo Monaka ambaye tarehe 25 mwezi huu wa Saba alifikisha miaka 113.

Hata hivyo historia inaonesha kuwa Japan inatajwa kama nchi yenye kusifika kuwa na watu wenye umri mkubwa zaidi duniani kwa kuwa watu wengi huishi zaidi ya miaka 65. Kufikia mwezi Februari 2018, watu 69,000 wameishi zaidi ya miaka 100, kulingana na Wizara ya Mambo ya Ndani na Mawasiliano nchini Japan, wanaume ni  9,000 na  60,000 kati yao ni wanawake.

 Aidha Mtu ambaye aliishi miaka mingi zaidi duniani kulingana na Guinness ni Jeanne Calment kutoka ufaransa,aliishi miaka 122 na siku 164. Aliaga dunia mwezi Agosti mwaka 1997.