Jumatatu , 10th Mar , 2025

Wizara ya Afya imesema kwamba Tanzania imethibitisha kuwa na wagonjwa wawili wa Mpox.

Mgonjwa wa Mpox

Taarifa hiyo imetolewa leo Machi 10, 2025 na kueleza kuwa Machi 7 Wizara ya Afya kupitia mifumo yake ya ukusanyaji wa taarifa na ufuatiliaji wa magonjwa ilipokea taarifa za uwepo wa wahisiwa wenye dalili za vipele usoni, mikononi, miguuni na sehemu nyingine za mwili dalili ambazo ziliambatana na homa, maumivu ya kichwa, vidonda kooni, maumivu ya viungo vya mwili ikiwemo misuli na mgongo ambapo kati ya wahisiwa hao mmoja ni dereva wa magari ya mizigo aliyetoka nchi jirani kwenda Dar es Salaam. 

"Baada ya kupokea taarifa za wahisiwa, sampuli zilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa kwa uchunguzi mnamo tarehe 9 Machi, 2025 uchunguzi wa kimaabara umethibitisha kuwa wahisiwa wawili wana maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Mpox, hivyo, hadi kufikia sasa jumla ya wahisiwa wawili wamethibitika kuwa na ugonjwa wa Mpox nchini," imeeleza taarifa ya Wizara ya Afya

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, inaendelea na ufuatiliaji, uchunguzi na utambuzi kubaini kama kuna wahisiwa wengine ili waweze kupatiwa huduma stahiki, chanzo cha ugonjwa huu ni wanyama jamii ya nyani, ambapo binadamu huweza kuupata kutokana na shughuli zinazoweza kusababisha kugusana na wanyama, majimaji au nyama za wanyama wenye maambukizi. Aidha, endapo binadamu akipata maambukizi hayo anaweza kumwambukiza mtu mwingine kwa kugusana moja kwa moja,".

Aidha Wizara ya Afya, imewahakikishia wananchi kuwa serikali imejipanga kudhibiti ugonjwa huo na hasa kutokana na uzoefu ilionao wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko.