Jumapili , 27th Aug , 2023

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ameshinda muhula wa pili na wa mwisho madarakani katika matokeo yaliyokataliwa na upinzani na kutiliwa shaka na waangalizi-Shirika la habari la Reuters limeripoti.

Mnangagwa ambaye alichukua wadhifa wa kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe baada ya mapinduzi ya jeshi mwaka 2017 alitarajiwa kuchaguliwa tena licha ya kuendelea kwa msukosuko wa kiuchumi nchini humo huku wachambuzi wakisema kuwa mchuano huo uliegemea upande wa chama cha ZANU-PF ambacho kimetawala nchi hiyo tangu uhuru na mwisho wa utawala wa wazungu wachache mwaka 1980.

Kwa mujibu wa tume hiyo, Mnangagwa alipata 52.6% ya kura kutokana na hesabu ya kura huku mpinzani wake mkuu Nelson Chamisa  wa chama cha  Citizens’ Coalition for Change akipata 44% na kusema kuwa chama chake  hakitatambua matokeo yoyote yaliyokusanywa kwa haraka bila kuthibitishwa ipasavyo.

Tarehe 23 Agosti, uchaguzi wa rais na wabunge ulifanyika nchini humo kisha upigaji kura uliongezwa kwa siku kutokana na ukiukaji wa utaratibu uliorekodiwa katika vituo kadhaa vya kupigia kura. 

Wagombea 11 walijitokeza kuwania kiti cha urais wa Zimbabwe akiwamo mkuu wa sasa wa nchi Mnangagwa na Ikatarajiwa kuwa Chamisa angekuwa mshindani wake mkuu. Hapo awali, Mnangagwa alishinda uchaguzi katika majira ya joto ya 2018.