Ijumaa , 12th Oct , 2018

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa ameguswa na kilio cha klabu ya Ndanda ya mkoani humo kwa kuichangia Sh 3,250,000 baada ya kukwama mkoani Singida kufuatia kukosa pesa ya kulipia gharama za malazi na safari ya kurudi.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa.

Ndanda fc imekwama mkoani humo tangu wiki iliyopita baada ya kucheza na wenyeji Singida United katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara, mchezo ambao Ndanda ilifungwa mabao 3-1.

Baada ya Afisa Habari wa klabu hiyo, Idrissa Bandari kuwaomba wadau wa mkoa huo na mashabiki kuichangia klabu hiyo kulipia gharama ilizotumia hadi sasa ambazo ni takribani Sh 4.2 millioni, ndipo mkuu huyo wa mkoa alipoamua kuichangia klabu hiyo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ndanda fc imemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa ambaye pia ni mlezi wao kwa jitihada zake za kuisaidia klabu hiyo kuhakikisha inasonga mbele .

Klabu hiyo inakamata nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara  mpaka sasa, ikiwa na alama nane baada ya kushuka dimbani michezo tisa. Imefungwa michezo mitano, imetoa sare michezo miwili na kushinda michezo miwili.

Ndanda inatarajia kurejea mkoani Mtwara kwaajili ya kuanza maandalizi ya mechi inayofuata ya ligi kuu itakayochezwa katika uwanja wake wa nyumbani wiki ijayo.