Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Injinia Evarest Ndikilo katika Mafunzo ya wadadisi wa utafiti wa kilimo wa mwaka 2016/17 yaliyofanyika mjini Kibaha.
"Nawaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wadadisi na wasimamizi wa takwimu, kwa kutoa taarifa sahihi kuhusiana na utafiti huu , napenda niwahakikishie wananchi kuwa kwa mujibu wa sheria ya takwimu namba tisa ya mwaka 2015, taarifa zitakazokusanywa zitatunzwa kwa usiri na zitatumika kwa shughuli za kitakwimu tu", alisema.
Ndikilo alisema sekta ya kilimo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi ambapo kwa mwaka 2016 ilichangia pato la taifa kwa asilimia 29.1 , na kati asilimia hiyo kilimo cha mazao kilichangia asilimia 15.5, mifugo, 7.7, misitu 3.9 na sekta ya uvuvi ilichangia asilimia 2.0.
"Sekta ya kilimo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wote wenye uwezo wa kufanya kazi hasa katika maeneo ya vijijini, kwa hivyo mafunzo haya ya leo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mipango ya kuboresha maisha ya watanzania walio wengi," alisema .
Hata hivyo Ndikilo alitoa agizo kwa watumishi hao kujifunza kwa bidii mafunzo hayo ya siku tano na kuwa watakaofaulu ndio watakwenda kufanya shughuli hiyo ya ukusanyaji wa data vijijini.
Naye mratibu wa mafunzo hayo kanda ya mashariki , mtakwimu kutoka makao makuu, Theresia Sagamilwa alisema mafunzo hayo yatawasaidia wadadisi kupata taarifa sahihi za kilimo ili kuisaidia serikali ijue maendeleo ya wakulima na mahitaji yao halisi ili kujua namna ya kuwasaidia.