
Kwa mujibu wa WHO, hatua hiyo imeathiri usambazaji wa dawa katika nchi saba za Afrika, zikiwemo Kenya, Lesotho, Sudan Kusini, Burkina Faso, Mali, Nigeria, na Haiti, ambazo zinaweza kuishiwa dawa ndani ya miezi michache ijayo.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kusitishwa kwa msaada huo kunaweza kufuta mafanikio ya miaka 20 katika kupambana na HIV.
Pia ameonya kuwa juhudi za kudhibiti magonjwa mengine kama polio, malaria, na kifua kikuu zimeathirika vibaya.
Ghebreyesus ameihimiza Marekani kuhakikisha kuwa inatoa muda wa mpito kwa nchi zilizoathirika ili ziweze kupata vyanzo mbadala vya fedha badala ya kusitisha msaada kwa ghafla, hatua ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya duniani.
Marekani kupitia kwa Rais wake Donald Trump ilitangaza mwezi huu kusitisha kutoa fedha za misaada kupitia miradi iliyokuwa chini ya Shirika lake la misaada la USAID, hali iliyoibua taharuki hasa kwa nchi nyingi za Afrika zinazotegemea fedha za ufadhili kushughulika na magonjwa kama Ukimwi.