Mkiniona naharibu alaumiwe Makinda- Spika Ndugai

Ijumaa , 11th Jun , 2021

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai amesema kuwa endapo ikitokea ameharibu katika kazi zake basi wa kulaumiwa ni Spika Mstaafu wa Bunge Mama Anne Makinda, kwani yeye ndiye aliyekuwa akimwongoza tangu awali.

Kushoto ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai, na kulia ni Spika wa Bunge Mstaafu Mama Anne Makinda

Kauli hiyo ameitoa Bungeni Dodoma, jana jioni Juni 10, 2021, wakati akimkaribisha Bungeni, na kuongeza kuwa Mama Makinda, amekuwa ni mwalimu wake kwa kipindi kirefu tangu alipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza.

"Mama Makinda amekaa humu Bungeni takribani miaka 40 hii rekodi siyo rahisi na yeye alikuja kama mbunge kijana, nilipoingia hapa Bungeni nilipangwa kwenye Kamati ya Ardhi Maliasili na Mazingira na yeye akawa ni Mwenyekiti wangu, miaka mitano iliyofuata yeye akawa Mwenyekiti wa Bunge mimi akaniachia kijiti kwenye kamati," amesema Spika Ndugai.

"Baadaye akawa Naibu Spika mimi nikawa Mwenyekiti wa Bunge yeye akawa Spika wa Bunge mimi nikawa Naibu Spika, ameenda kustaafu nimekuwa Spika kwa hiyo mimi huwa nafuata mguu wake anapotoa mimi naweka sasa kwa vile alishastaafu na mimi nafuatia nitakuja kuwaambia huko mbele, namshukuru sana Mama kwa malezi mkiniona naharibu alaumiwe yeye maana yeye ndiyo mwalimu wangu kila hatua," ameongeza Spika Ndugai.