Jumatatu , 26th Mei , 2014

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro amesema miradi ya maendeleo inayozinduliwa katika mbio za mwenge haiwezi kuwa na manufaa endapo itagubikwa na rushwa.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro (Kushoto) akipokea mwenge wa uhuru katika mkoa wa Mbeya kutoka Rukwa.

Mkuu wa mkoa wa mbeya Abbas Kandoro amesema miradi ya maendeleo ya wananchi yenye thamani ya zaidi ya sh. bil. 15. 4 inayozinduliwa na mwenge katika mkoa wa Mbeya inaweza kuwa na manufaa kwa jamii iwapo haitagubikwa na vitendo vya rushwa na ubadhilifu.

Mkuu huyo wa mkoa akizungumza na wananchi wa wilaya ya Momba baada ya kupokea mwenge ukitokea mkoani Rukwa amesema ni dhahili kwamba palipo na rushwa hakuna maendeleo endelevu.

Amesema wakati serikali ikiendelea kupambana na vitendo vya rushwa, ni wajibu wa wananchi kutoa taarifa zinazoashiria kuwepo kwa ubadhilifu na ufujaji wa fedha katika miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

Naye kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa bi. Rachel Kasanda amesema hakuna faida ya Tanzania kung'ara kimataifa kama wananchi wake wataendelea kuwa masikini wakati nchi ina utajiri mkubwa wa rasimali nyingi zisizo nufaisha wananchi wake.

Zaidi ya miradi 100 inawekewa mawe ya msingi, kuzinduliwa, na kukaguliwa na mwenge katika mkoa wa Mbeya, miradi hiyo inahusisha wanawake na vijana katika afya, kilimo, elimu, ufundi na mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji.