Jumanne , 23rd Sep , 2025

Huko Roma, watu wapatao 20,000 walikusanyika mbele ya kituo kikuu cha treni cha Termini, kulingana na polisi wa eneo hilo, wengi wao wakiwa wanafunzi, wakipaza sauti “Palestine Huru!” na kushikilia bendera za Palestina. Wengine waliandamana kupitia Ukumbi wa Colosseum.

Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni amewashutumu waandamanaji aliowaita kuwa ni wa bandia ambao walipambana na polisi wakati migomo na maandamano yaliposababisha ghasia katika miji kadhaa jana Jumatatu, Septemba 22 ambapo makumi ya maelfu ya watu waliandamana kote Italia ikiwa ni hatua ya kushutumu mauaji ya kimbari yanayoedelea huko Gaza.

Polisi wa kutuliza ghasia walirusha mabomu ya machozi kujaribu kuwatawanya waandamanaji katika kituo kikuu cha Milan jana Jumatatu huku waandamanaji, wengine wakiwa wamevalia nguo nyeusi na wengine wakipeperusha bendera ya Palestina, wakitumia nguzo kuvunja dirisha kwenye kituo hicho na kurusha vitu. Zaidi ya watu 10 walikamatwa huko Milan na maafisa wa polisi wapatao 60 walijeruhiwa.

Vyama vya chini vya Italia, ambavyo vinawakilisha mamia ya maelfu ya watu kutoka kwa walimu wa shule hadi mafundi chuma, vilitoa wito wa mgomo wa jumla wa masaa 24 katika sekta za umma na za kibinafsi, ikiwemo sekta ya usafirishaji wa umma, gari moshi, shule na bandari hatua ambayo ilisababisha usumbufu kote nchini humo, na kucheleweshwa kwa muda mrefu kwa treni za kitaifa na usafiri mdogo wa umma katika miji mikubwa.

Katika bandari ya Venice, polisi walisambaza maji ya kuwasha kusaidia kuvunja maandamano. Wafanyakazi pia walifanya maandamano katika bandari katika miji ya Genoa, Livorno na Trieste. Wafanyakazi wa bandarini walisema wanatafuta namna ya kuizuia Italia isitumike kama kituo cha kupeleka silaha na vifaa vingine kwa Israel ambavyo vinatumika katika vita vyake huko Gaza.

Waandamanaji walisimamisha trafiki kwenye barabara kuu karibu na mji wa Bologna kabla ya kutawanywa na maji ya kuwasha, huku huko Roma makumi ya maelfu walikusanyika nje ya kituo kikuu cha treni kabla ya maandamano ambayo yalifunga barabara kuu ya mzunguko. Katika jiji la kusini la Naples, kulikuwa na mapigano na polisi huku umati wa watu ukilazimisha kuingia kwenye kituo kikuu cha reli.

Bi Meloni amesema ghasia na uharibifu huo hauhusiani na mshikamano na haitabadilisha hata kitu kimoja katika maisha ya watu wa Gaza, lakini itakuwa na matokeo madhubuti kwa raia wa Italia, ambao wataishia kuteseka na kulipa uharibifu unaosababishwa na majambazi hao.