Jumatano , 11th Aug , 2021

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limemkamata mwanaume mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa akiwa kwenye mazingira ya kutatanisha, hatua hiyo imekuja baada ya wananchi kudai kwamba amekuwa akiingia katika nyumba zao majira ya usiku kwa mtindo wa kuteleza na kisha kutokea dirishani.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo

Taarifa ya kukamatwa kwa mtu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa imetolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo, na kusema kwamba mtu huyo alikamatwa majira ya saa 9:00 alfajiri ya Agosti 10, 2021.

Hivi karibuni wananchi wa eneo la kwa Morombo mkoani Arusha, walilalamikia uwepo wa mwanaume anayeingia majumbani mwao akiwa amejipaka mafuta mwili mzima yaani mtindo wa teleza na kwamba baada ya wananchi kumkamata walimkuta akiwa na nguo za ndani za wanawake.

Mmoja wa wanawake ambao wanadai kwamba mwanaume huyo alimbaka mdogo wake wa miaka 14 na kumjeruhi, akizungumza kwa uchungu alisema kwamba analishangaa Jeshi la Polisi kwa kumshikilia mwanaume huyo lakini lengo lake yeye ni kumuona ili ajue kama ni binadamu wa kawaida ama anafanana na nini.