Jumatano , 23rd Dec , 2020

Mifuko 70 ya mawe ya madini ya dhahabu imekamatwa mkoani Simiyu yaliyokuwa yakitoroshwa kinyume cha sheria kutoka mgodi wa EMJ wilayani humo, ambapo watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Pichani: mfano wa jiwe la dhahabu (picha kutoka mtandaoni)

Afisa madini wa mkoa wa Simiyu, Oscar Kaloa amesema mawe hayo ya madini ya dhahabu wameyakamata usiku kupitia operesheni yake,  yakisafirishwa kwa njia ya magendo kutoka mgodi huo kwenda Mjini Bariadi huku yamepakiwa kwenye trekta.

“Wakati wa doria yetu tukitoka maeno ya  Dutwa kuelekea Bariadi mjini mida ya karibu saa 3:25 usiku, tukaona trekta mmoja ikiwa na mifuko ikielekea Bariadi mjini tukaisimamisha tukataka ituonyesha kibali ya walichokibeba, wakatoa kibali ambacho kilionyesha ni mifuko 4 ambayo ilikuwa inatoka mgodi wa EMJ  na tulipoenda kwenye trela na kuikagua tukabaini ni mifuko takribani 70 na haina nyaraka zozote” amesema Kaloa

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga, amewaonya wanaotorosha madini wilayani kuwa watachukua hatua kali pamoja na kuagiza kukamatwa wanaotoza ushuru usiokuwa rasmi.