Jumatano , 27th Aug , 2025

Korea Kusini imepitisha muswada wa kupiga marufuku matumizi ya simu za mkononi na vifaa janja wakati wa masomo darasani 

Korea Kusini inakuwa nchi ya hivi karibuni zaidi kuzuia matumizi ya simu miongoni mwa watoto na vijana.
Sheria, ambayo itaanza kutumika kuanzia mwaka ujao wa masomo mnamo Machi 2026, ni matokeo ya juhudi za pande mbili za kuzuia uraibu wa simu janja, kwani utafiti zaidi unaangazia madhara yake.

Wabunge, wazazi na walimu wamesema kuwa matumizi ya simu janja yanaathiri utendaji wa wanafunzi kitaaluma na kuwaondolea muda ambao wangetumia kusoma.

Marufuku hiyo ina wakosoaji wake, ikiwa ni pamoja na wanafunzi, ambao wanahoji jinsi itakavyofanya kazi, athari zake pana na ikiwa inashughulikia sababu kuu ya uraibu.

Muswada huo ulipitishwa kwa kishindo Jumatano mchana, kwa kura 115 za ndio kati ya wanachama 163 waliohudhuria.

Shule nyingi za Korea Kusini tayari zimetekeleza aina fulani ya marufuku ya simu hizo.
Na wao si wa kwanza kufanya hivyo. Baadhi ya nchi kama vile Finland na Ufaransa zimepiga marufuku simu kwa kiwango kidogo, zikitumia kizuizi hicho kwa shule za watoto wadogo pekee.

Nyingine kama Italia, Uholanzi na China zimezuia matumizi ya simu katika shule zote.

Lakini Korea Kusini ni miongoni mwa wachache wanaoweka marufuku hiyo kisheria. Watoto siku hizi "hawaonekani kuweka simu zao chini," anasema Choi Eun-young, mama wa mtoto wa miaka 14 huko Seoul.

Hatahivyo, si watoto tu. Takriban robo ya watu milioni 51 nchini wanategemea sana simu zao, kulingana na utafiti wa serikali wa 2024.