
Majaliwa ameyasema hayo wiki hii alipozungumza na madaktari wa hospitali ya Ruvuma kwamba amefurahishwa sana na utaratibu wao wa kuandaa chumba maalum chenye madaktari wawili kwa ajili ya kuwahudumia wazee wanaofika hospitalini hapo kupata huduma ya afya jambo ambalo limeondoa adha kwa wazee hao kukaa muda mrefu wakisubiri huduma na wakati mwingine bila mafanikio.
''Hosptali zote nchini ziige mfano huu wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma kwa kutenga dirisha maalum kwa ajili ya kuhudumia wazee kama ilivyo agizo la serikali na wasitozwe malipo yoyote'' Alisisitiza Waziri Majaliwa.
Aidha waziri mkuu ameongeza kuwa hata wazee wanapokwenda kuchukua dawa wapewe kipaumbele maalumu ili wasisubiri muda mrefu,pia kibali cha kutibu wazee bure katika hospitali kiwe cha kudumu na kiheshimiwe na wote.
Mara kadhaa serikali imekuwa ikitoa tamko kuhusiana na kutibu wazee na watoto chini ya umri wa miaka mitano bure hapa nchini jambo ambalo limekuwa halitekelezwi kwa vitendo na kusababisha malalamiko na adha kubwa kwa wagonjwa wanaokwenda kupata huduma za afya hapa nchini.