Ijumaa , 27th Jan , 2023

Samson Masalu (18) amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza kwa kosa la ubakaji, kwani amekuwa akimbaka msichana mwenye umri wa miaka 17 na kumsababishia kushindwa kuripoti shule ya sekondari Bujiku Sakila aliyopangiwa kujiunga kidato cha kwanza.

Samson Masalu

Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Kwimba John Jagadi, Mwendesha Mashtaka wa serikali Robert Mwanakatwe, ameiambia mahakama hiyo kuwa Masalu anadaiwa kuishi na binti huyo tangu Desemba 2022, na kuwalipa wazazi wa binti huyo mahari ya ng’ombe saba hadi tarehe 23 ya mwezi huu wa kwanza polisi walipombaini na kumkamata mwanaume huyo huku wazazi wa binti huyo wakikimbia kusikojulikana.

Aidha Mwendesha Mashtaka huyo wa serikali amesema mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la ubakaji kwa mujibu wa kifungu cha 130 kidogo cha pili E na kifungu 131 kidogo cha kwanza cha sheria ya adhabu sura ya 16 marekebisho ya mwaka 2022.

Baada ya kusomewa shtaka lake la ubakaji mshtakiwa huyo amerudishwa rumande katika gereza la wilaya ya Kwimba hadi tarehe sita ya mwezi wa pili mwaka huu shtaka hilo litakapotajwa tena.