Alhamisi , 12th Sep , 2019

Fikra kwamba bodaboda ndizo zinaongoza kwa kusababisha vifo na majeruhi kutokana na ajali za barabarani, hazilandani na uhalisia wa takwimu za hivi karibu za ajali za barabarani.

Ajali za barabarani

Kinyume chake ni kwamba idadi ya vifo vya ajali za barabarani hapa nchini zinazosababishwa na magari binafsi imezidi kuongezeka kwa kasi katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa mwaka 2019 na sasa inazidi hata vifo vya ajali zitokanazo na pikipiki maarufu kama bodaboda, ambazo ndizo zilikua zikiongoza kwa kusababisha vifo.

Takwimu za Jeshi la Polisi katika kipindi cha miezi sita Januari - Juni 2019 zinaonesha kuwa magari binafsi ndiyo yamekuwa vinara wa kusabisha ajali zinazosababisha vifo na hata majeruhi.

Wadau wa usalama barabarani wanaonya kuwa hali inaweza kuwa mbaya zaidi kama hatua za haraka hazitachukuliwa kwani kwa mujibu wa takwimu rasmi za Jeshi la Polisi (Januari mpaka Juni 2019), magari binafsi yamesababisha ajali 528, vifo 222 na majeruhi 453, kwa wastani; Kila siku magari binafsi husababisha ajali tatu, kifo cha mtu mmoja mpaka wawili na majeruhi wawili. 

Kwa miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu pikipiki zimesababisha ajali 334, vifo 176, majeruhi 319, kwa wastani pikipiki zinahusika katika ajali mbili kila siku na kusababisha kifo cha mtu mmoja tu, na mmoja mpaka wawili. Takwimu zingine zinaonesha mabasi ya abiria yakipata ajali 103, na kusababisha vifo 61 na majeruhi 195 katika kipinidi hicho. 

Pia ripoti hiyo inaonesha kwamba malori yalihusika katika ajali 167, na kusababisha vifo vya watu 130 na majeruhi 142, wakati daladala za abiria zilipata ajali 143, na kusababisha vifo 89 na majeruhi 268. 

Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Deus Sokoni, amesema wanachukua hatua mbalimbali kudhibiti ajali za magari binafsi ikiwemo kufungia leseni za madereva wanaosababisha ajali kwa uzembe, na kujihusisha na ulevi, mwendokasi na makosa mengineyo.

Aidha ameeleza kuwa wanataraji kufanyika kwa mabadiliko ya kisheria ambayo yatasaidia kudhibiti magari binafsi katika masuala mbalimbali ikiwemo mwendokasi, ulevi pamoja na ufungaji wa mikanda. “tupo kwenye mchakato wa mabadiliko ya sheria ili iwe lazima kwa abiria wote wanaopanda magari binafsi kufunga mikanda. Kwa sasa anayelazimika kisheria ni dereva na abiria wa mbele tu,” anasema ASP Sokoni.

Utafiti wa WHO unasema kufunga mkanda wa usalama humsaidia abiria wa mbele kujikinga na madhara ya ajali kwa asilimia 40 mpaka 50, na asilimia 50-75 kwa abiria waliokaa viti vya nyuma.

Henry Bantu ambaye ni Mkurugenzi wa Safe Speed Foundation, asasi ya kiraia inayojihusisha na masuala ya usalama barabarani anasema magari binafsi kuwa vinara katika matukio ya ajali za barabarani kunasababishwa na mambo mengi ikiwemo udhibiti hafifu wa magari hayo pamoja na mfumo mbovu wa utolewaji wa leseni za udereva.

Magari binafsi yakipata ajali hayatangazwi sana, inachukuliwa kama jambo binafsi lakini basi la abiria likipata ajali, nchi nzima itatangaziwa, pia hawa madereva wa magari binafsi wanamudu kununua magari na hata kutoa fedha ili kupata leseni kwa njia wanazozijua".

Ni lazima yafanyike mapinduzi ili kudhibiti ajali za magari binafsi, nguvu kubwa sana inatumika kudhibiti na kufuatilia magari ya abiria na bodaboda kuliko kukagua na kufuatilia magari binafsi. Wananchi pia lazima wajue kuwa usalama barabarani ni jukumu lao na waone haja ya kupita mafunzo kamili ili kupata leseni halali ili wawe salama barabarani,” anasisitiza.

Ripoti ya usalama barabarani ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) iliyotolewa mwaka 2018, inabainisha kuwa Sheria za Tanzania zina upungufu katika kudhibiti usalama barabarani, ikiwemo kuruhusu kiwango kikubwa cha ulevi kwa madereva bila kujali uzoefu wa dereva katika kazi husika.

Tanzania imeweka ukomo wa kilevi kuwa ni 0.08g/dl lakini WHO inaeleza kuwa dereva mwenye kiwango hiki cha ulevi anakua hatarini kupata ajali mara nne zaidi ya yule ambaye hajatumia pombe kabisa. WHO pia wanashauri kuwa ni vizuri ukomo wa ulevi ukawa ni 0.05g/dl kwa madereva wazoefu na 0.02g/dl kwa madereva wapya wasio na uzoefu.

Kwa mujibu wa taarifa za polisi nchini, zaidi ya ajali 2,250 zimerekodiwa kuwa zilitokana na ulevi katika kipindi cha mwaka 2006 mpaka 2017 huku magari binafsi yakitajwa kuhusika zaidi kwenye ajali hizo. Takwimu hizi ni wastani kutokea kwa ajali 15 kila mwezi kutokana na  ulevi.

Salha Rajabu, ambaye ni dereva wa gari binafsi na mkazi wa Bunju jijini Dar es Salaam anasema ajali za magari binafsi ni nyingi kutokana na magari hayo kuzidi kuongezeka, lakini pia baadhi ya ajali hasa zinazotokea wakati wa usiku zinasababishwa na ulevi, uchovu na ukaidi wa makusudi wa sheria kutokana na kupungua kwa askari barabarani.

Usiku askari wanapungua barabarani, hasa maeneo ya makutano na hata njiani ambako mchana huwa wanakuwepo kuongoza magari, kupima mwendokasi na kuangalia wanaotanua au kutozingatia alama za barabarani kama pundamilia, lakini jioni mpaka usiku panakuwa huru. Watu wanakimbia sana na wengine wanakua wametoka kazini wakiwa wamechoka au wamepitia maeneo ya vilevi,” anaeleza Salha.

Irene Msellem, mdau wa usalama barabarani anatoa mtazamo wake kuhusu ajali za magari binafsi akisema magari yenye uzito chini ya tani 3.5 hayajawekewa ukomo wa mwendo kisheria, kwani yanatakiwa kwenda kilometa 50 kwa saa katika maeneo ya makazi, lakini maeneo yasiyo na makazi wala vibao vya kuelekeza mwendo wanaweza kwenda mwendo wowote ambao dereva ataona unafaa.

Wadau tunapendekeza kuwa kama ilivyo kwa mabasi na magari mengine makubwa yanavyoadhibiwa kwa kuzidisha kilometa 80 kwa saa, uwekwe pia ukomo katika magari binafsi ambao unaweza kuwa kilometa 100 kwa saa,” anasisitiza.