Jumapili , 6th Aug , 2023

Wafugaji wa vipepeo wa tarafa ya Amani Wilayani Muheza Mkoani Tanga wamemuomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutazama upya zuio la serikali la kusafirisha vipepeo wanavyovizalisha kwajili ya shughuli za utalii na kuviuza nje ya nchi.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wafugaji hao wamesema biashara hiyo wamekuwa wakiifanya kwa miaka mingi iliyopita ikiwasaidia kujikwamua kiuchumi lakini baada ya zuio hilo hali zao za kiuchumi zimebadilika na hivyo kushindwa kuendesha maisha yao.

Diwani wa kata ya kisiwani Shaban Chewaja amesema hivi karibuni walikwenda mjini Dodoma na kukutana na katibu mkuu wa wizara ya maliasili na utalii ambaye walifikisha hoja zao ambapo aliwaahidi kufikisha kilio cha wananchi hao kwa Rais Dkt Samia na kisha kuwarejeshea majibu. 

Mwezi Machi kamati ya kudumu ya bunge ya uwekezaji na mitaji ya umma (PIC) ilijia juu katazo hilo la kusafirisha viumbe hai nje ya nchi changamoto ambayo hadi hivi sasa bado haijapatiwa ufumbuzi kwa wafugaji hao
Serikali ilitoa katazo hilo baada ya kuingia dosari ya kusafirisha viumbe wengine zaidi ya vipepeo hatua ambayo iliathiri kwa kiwango kikubwa wafugaji hao, zuio ambalo lilitolewa mwaka 2019.