Jumapili , 17th Sep , 2023

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete, amewatahadharisha watumishi wa umma kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa maarufu kwa jina la kausha damu, huku akisisitiza kuwa mikopo hiyo imekuwa ikidhalilisha na kutweza utu wao kwenye jamii.

aibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Ridhiwani Kikwete

Naibu Waziri Kikwete ametoa tahadhari hiyo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Busega mkoani Simiyu wakati akihitimisha ziara yake aliyoianza mapema wiki hii mkoani Mara.

Amesema mikopo hiyo imewafanya baadhi ya watumishi wa umma kuathirika kisaikolojia na kushindwa kufika katika vituo vya kazi na hivyo kuathiri utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Amefafanua kuwa mikopo hiyo ambayo huchukuliwa kwenye taasisi za kifedha zisizotambulika imekuwa na riba kubwa ambayo huwapelekea watumishi wengi kushindwa kuwasilisha marejesho na hivyo kupelekea kuuzwa kwa nyumba au vitu vya thamani wanavyo vimiliki.

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Kikwete amewataka watumishi kuanza kutumia mfumo mpya wa kieletroniki wa kukopa (e-loans) ulioanza kutumika kuanzia Septemba 1, 2023  ambao unamuwezesha mtumishi wa umma kuomba mkopo pasipo kufika kwenye taasisi ya kifedha au tawi la benki.

Amesema mfumo huo umeanzishwa na Ofisi ya Rais -  UTUMISHI na Utawala Bora ili kumsaidia mtumishi kupata mikopo katika taasisi za kifedha zinazotambulika na mwajiri ili kumuepusha kukopa sehemu ambazo humpelekea kunyang'anywa kadi ya benki.

Aidha, Mhe.Kikwete amewataka watumishi hao kujenga nidhamu ya matumizi ya pesa wanazopata kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao ya  baadaye baada ya kustaafu.