
Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe.
Wakili Mkuu wa Serikali, Paul Kadushi, amesema hayo leo Januari 3, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
"Shauri limekuja kwa ajili ya kutajwa na kwa kuwa kuna amri ya kusitisha mwenendo wa kesi hii katika Mahakama ya Hakimu, hivyo tunasubiri uamuzi ya Mahakama ya Rufaa. Hivyo kutokana na hali hiyo, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amedai Kadushi.
Baada ya Wakili Kadushi kueleza hayo, wakili wa utetezi, Profesa Abdallah Safari ameomba kujua endapo upande wa mashtaka kama wamewasilisha hati ya dharura katika Mahakama ya Rufaa. Akijibu hoja hiyo, Kadushi amedai upande wa utetezi hawana uhalali wowote wa kuhoji suala hilo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mashauri aliutaka upande wa utetezi kwenda kuhoji suala hilo Mahakama ya Rufaa. Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, 2019, itakapotajwa.
Mbowe na Matiko wanasota mahabusu baada ya Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana yao Novemba 26,2018 kwa kukiuka masharti ya dhamana, ambapo waliamua kukata rufaa Mahakama Kuu lakini iliwekewa pingamizi baada ya upande wa mashtaka kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya na Katibu wa CHADEMA Zanzibar, Salum Mwalimu.
Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya February Mosi na 16, 2018 jijini Dar es Salaam.