Alhamisi , 6th Aug , 2015

Kasi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukihama chama hicho imepamba moto baada ya madiwani 18 wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, kutangaza nia yao jana Jijini Arusha.

Elias Ngorisa, katibu wa fedha na uchumi wa CCM Wilaya ya Ngorongoro pamoja na madiwani kadhaa wamejiunga CHADEMA na kupokelewa na Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari

Madiwani hao waliwakilishwa ofisi za Chadema Mkoa wa Arusha leo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Elias Ngorisa aliyeambatana na Diwani wa Kata ya Engusero Sambu, Kagil Mashati Ngukwo, ambaye pia alikuwa Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM Wilaya ya Ngorongoro.

Pamoja nao walikuwepo wazee wa mila wa Kabila la Wamasai (malaigwanani) Laurence Ngorisa na Lekakui Oleiti, wote kutoka Engusero Sambu.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, ndiye aliyewapokea makada hao na kuwapatia kadi za Chadema.

Akizungumza baada ya kupokea kadi, Elias Ngorisa, amesema wapo madiwani 18 kati ya 28 ambao tayari wamechukua kadi za Chadema na kuondoka CCM na watatetea nfasi zao kupitia Chadema katika uchaguzi wa oktoba mwaka huu.

Amesema yapo mabadiliko makubwa na Watanzania hawana budi kuyakubali na ameshawishika kwa dhati kabisa kubadilisha mwelekeo toka CCM kwenda Chadema.

Kwa upande wake, Diwani Ngukwo, amesema, amekihakama chama hicho kwa sababu anahitaji mabadiliko na anaamini wengi watawafuata ili ili waweze kuondokana na manyanyaso mengi ya Loliondo wanayopata.

Mapema Mbunge Nassari amesema Chadema itaendelea kuwapokea makada wa vyama vyote watakaovihama vyama vyao na akaelezea kuwa wana timu kubwa kule Ngorongoro ambayo itawafuata.