Rais Kikwete akiwa na baadhi ya viongozi kutoka nje, katika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete usiku wa jana, Jumapili, Aprili 27, 2014 alikamilisha saa 24 za mikutano mfululizo na baadhi ya viongozi na wajumbe maalum walioziwakilisha nchi zao katika sherehe za Miaka 50 ya Muungano.
Kilele cha Sherehe hizo za kufana kilifanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maelfu kwa maelfu ya wananchi na mamia ya wageni kutoka nchi mbali mbali duniani ambao Tanzania iliwaalika kushiriki sherehe hizo.
Katika mikutano hiyo, Rais Kikwete alikutana na Rais Mstaafu wa Zambia Mheshimiwa Rupiah Banda, Rais Mstaafu wa Namibia Mheshimiwa Sam Nujoma na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la China Mheshimiwa Chen Changzhi.
Wengine ambao Rais Kikwete alikutana nao ni Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Algeria Mheshimiwa Abdulkadir Messahel, Waziri wa Serikali za Mitaa wa Angola Mheshimiwa Bernito de George Beltazar, Waziri wa Mambo ya Ndani na Wanyamapori wa Sudan Kusini Mheshimiwa Aley Anjieng Aleu na Makamu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mheshimiwa Geraldine Fraser - Moleketi.
Rais Kikwete alikamilisha mikutano hiyo kwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Rupia Banda, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Zambia, ambaye alikutana naye Ikulu, Dar Es Salaam, usiku wa jana.
Mheshimiwa Banda alimpongeza Rais Kikwete kwa kuandaa sherehe nzuri na za kuvutia sana na hasa onyesho la halaiki ya watoto pamoja na gwaride na maonyesho ya silaha za kijeshi.
Mapema asubuhi ya jana, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Sam Nujoma, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Namibia, ambaye alieleza furaha yake ya kurejea tena Tanzania ambako aliishi wakati wa kutafuta uhuru wa Namibia.
Mzee Nujoma alimweleza Rais Kikwete kuwa sherehe za Jumamosi zimethibitisha kuwa Tanzania inao uwezo wa kutosha wa kijeshi wa kukabiliana na shambulio lolote kwa Bara la Afrika kutoka nje ya bara hilo.
“Maonyesho yale ya kijeshi yamethibitisha kuwa Tanzania inao uwezo wa kukabiliana na kuzuia shambulio lolote dhidi ya Bara la Afrika ambalo linapitia upande huu wa Bahari ya Hindi – mnalo jeshi lenye nguvu la maji, jeshi lenye nguvu la anga na jeshi lenye nguvu la nchi kavu,” alisema Mzee Nujoma.
Aidha, Rais Kikwete na Mzee Nujoma walizungumzia namna ya kuboresha na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Namibia na Tanzania.
Mzee Nujoma pia alimweleza Rais Kikwete wazo la Serikali ya Namibia na chama tawala cha nchi hiyo cha SWAPO la kutaka kuishawishi Serikali ya Tanzania kukubali na kutoa ruhusa kwa SWAPO kujenga mnara na sanamu ya heshima ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na kuuweka Kongwa, Mkoa wa Dodoma, ambako SWAPO walianzia maisha yao katika Tanzania wakati wanaendesha vita ya ukombozi dhidi ya makaburu.
Katika mkutano wake na Rais Kikwete, Mheshimiwa Changzhi alieleza kuwa ilikuwa heshima pekee kwake kuhudhuria sherehe hizo za miaka 50 na kumwalikisha Rais Xi Jingping na kuwa sherehe hizo zilikuwa za mvuto uliokuwa wa kawaida kijeshi na kiraia.
Naye Rais Kikwete aliishukuru China kwa mchango wake mkubwa katika shughuli za maendeleo kwa miaka 50 iliyopita tokea nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano mwaka 1964.