Alhamisi , 21st Sep , 2023

Hispania kupitia wakala wake wa bima (Export Credit Agency - ECA), imeonesha nia ya kushiriki katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa kutoa mikopo, dhamana ya mikopo na Bima kwa kampuni za nchi hiyo zitakazojenga reli hiyo kuanzia Makutopora hadi Mwanza na kipande cha kuanzia

Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii, Xiana Mendez akiwa na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba

Tabora - Kigoma hadi Malagarasi.

Ahadi hiyo imetolewa mjini Madrid, Hispania, na Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Utalii, Xiana Mendez, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Dkt Mwigulu Nchemba, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, ukiwemo ujenzi wa mradi huo mkubwa wa SGR.

Amesema kuwa Hispania inatambua umuhimu wa mradi huo kwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi hiyo kwa kuwa kukamilika kwake kutaongeza mnyororo wa thamani wa uwekezaji na biashara na kuwa Kituo cha biashara katika Ukanda wa Afrika.

Bi. Mendez ameusifu uchumi imara wa Tanzania pamoja na uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji, hatua ambayo imezifanya kampuni nyingi kutoka nchi hiyo kutaka kushiriki katika uwekezaji na ujenzi wa miradi ya miundombinu itakayochochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania, ikiwemo pia nishati jadidifu.

Aliahidi pia kuwa nchi yake itafungua ofisi jijini Dar es Salaam kutokana na kuongezeka kwa uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili kwa ajili ya kurahisisha shughuli hizo za kibiashara.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Hispania kupitia Wakala wake wa Bima, kwa kuonesha nia ya kuziwezesha kampuni za Hispania zitakazofanya shughuli zake za biashara na ujenzi wa miundombinu mbalimbali nchini Tanzania, ukiwemo mradi wa reli, mikopo, dhamana ya mikopo na bima kwa kampuni zinazoshiriki katika ujenzi wa miradi nje ya nchi hiyo. 

"Ushiriki wa Wakala wa Bima wa Hispania (Export Credit Agency-ECA), katika kutekeleza mradi huo wa kimkakati ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na kwa ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu kati ya Hispania na Tanzania, na kwa maendeleo ya wananchi kwa ujumla," amesema Dkt Nchemba

Alisema kuwa katika kuimarisha uhusiano na maandalizi ya kutekeleza ufadhili huo wa SGR, Mkandarasi ametafuta kampuni 12 za Kihispania zitakazosambaza vifaa vitakavyotumika kujenga reli hiyo na kumwomba Naibu Waziri huyo na Serikali yake kwa ujumla, kuzishawishi kampuni nyingi zaidi kutoka nchini humo kujitokeza kushiriki katika ujenzi wa mradi huo.

Zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.24 zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha tatu, nne na cha tano kinachoanzia Makutopora hadi Mwanza, na ziara ya Mhe, Dkt Nchemba na ujumbe wake katika nchi za Ulaya ni kukutana na kufanya majadiliano na Taasisi za Fedha na wadau mbalimbali, kutafuta fedha za kugharamia ujenzi wa Reli hiyo.