Jumapili , 19th Apr , 2015

Shirika lisilo la kiserikali la Hakielimu limesikitishwa na jinsi serikali isivyopeleka kwa wakati pesa za ruzuku kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kiasi cha kusababisha mzigo wa michango isiyo ya lazima mwa wazazi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa HakiElimu, Godfrey Boniventura (kulia) akiwa na Msemaji wa shirika hilo Elisante Kituro.

Aidha, shirika hilo limesema kuchelewa au kutopelekwa kwa pesa za ruzuku kwa kiasi fulani kumechangia kushuka kwa kiwango cha elimu nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hakielimu, Godfrey Boniventura amesema hali hiyo imebainika kufuatia ufuatiliaji uliofanywa na shirika hilo katika mikoa na wilaya kadhaa nchini ambapo kwa wastani shule mpaka sasa zimepokea shilingi zisizozidi mia nane, kati ya shilingi elfu kumi anazostahili kupata kila mwanafunzi, kiwango ambacho ni sawa na asilimia tisa tu ya pesa yote.

Wilaya 10 ambako ufuatiliaji wa hali ya ruzuku ya mwanafunzi umefanyika ni pamoja na Kilosa, Kilwa, Arusha vijijini, Iramba, Bariadi, Ukerewe, Serengeti, Kigoma Vijijini, Manispaa ya Tabora ambapo jumla ya shule 40 za msingi na 40 za sekondari zilihusishwa.