Jumatano , 2nd Aug , 2023

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imesema ipo tayari kushirikiana kikamilifu na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kwa kutumia umeme gridi ya Taifa baada ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme na mradi wa kupeleka umeme katika migodi ya kampuni hiyo kukamilika.

Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo akichangia mjadala wa nishati kupitia Jukwaa la fikra la Mwananchi.

 

Pia imeipongeza Tanesco na wizara ya nishati kwa kuja na mpango mkakati wa miaka 10 ambao utaliwezesha shirika hilo kuanzisha vyanzo vipya vya nishati endelevu kwani ni jambo litakalolisaidia Taifa kutimiza lengo namba saba la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) linalozungumzia matumizi ya nishati inayofikika, ya gharama nafuu, endelevu na ya kisasa kwa wananchi wake.
 
Hayo yameelezwa jana na Makamu Rais wa AngloGold Ashanti- GGML anayeshughulikia miradi endelevu kwa upande wa Ghana na Tanzania, Simon Shayo wakati akichangia mjadala wa nishati kupitia Jukwaa la fikra la Mwananchi.
  
"Ni hatua kubwa kwa Tanesco kutafsiri kwenye mkakati wake lile lengo namba saba," alisema.
   
Awali akizindua mpango huo mkakati wa Tanesco, Waziri wa Nishati, Januari Makamba aliwataka wananchi wawe na subira wakati shirika hilo linafanya mageuzi ya utendaji kazi wake.
Alisema Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuipa mtaji TANESCO ili itekeleze mipango yake kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi na Afrika kwa ujumla.
 
Naye Mkurugenzi wa TANESCO, Maharage Chande alisema shirika hilo linakusudia kuendelea na mipango yake ya kuboresha huduma kwa wateja wake, kupitia miradi mbalimbali ikiwemo wa kufua umeme katika Bwawa la Julius Nyerere, ambao unatarajia kuanza kuzalisha umeme Juni 2024.