Jumatano , 27th Apr , 2016

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Richard Sezibera, amesema katika kipindi chake jumuiya hiyo imekuwa na mafanikio makubwa katika nyanja tofauti za kimaendeleo licha ya kuwepo kwa changamoto za kiusalama.

Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Bw. Libarat Mfumukeko, kutoka nchini Burundi

Dkt.Sezibera amesema hayo jana Jijini Arusha wakati akikabidhi ofisi kwa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya hiyo Bw. Libarat Mfumukeko, kutoka nchini Burundi baaada ya Dkt. Sezibera kumaliza muda wake wa kipindi cha miaka mitano.

Dkt. Sezibera amesema kuwa jumuiya imepiga hatua za kimaendeleo katika miundombinu, Umoja wa Forodha, Pasi za Kusafiria za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na soko la pamoja lakini suala la usalama la nchini Burundi limebaki changamoto.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya hiyo, Balozi Augustino Mahiga, amesema kuwa sektretarieti ina jukumu la kuharakisha uanachama wa Sudan ya Kusini ili kushiriki katika nafasi mbalimbali za uongozi katika jumuiya hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu huyo Mpya Bw. Libarat Mfumukeko amesema katika uongozi wake jumuiya itazingatia malengo makuu na kusimamia masuala yote kikamilifu.

Sauti ya Aliekua Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Richard Sezibera akizungumzia changamoto za EAC.
Sauti ya balozi Augustino Mahiga, akizungumzia mchakato wa Sudan kusini kuingia katika mchakato wa kiutawala